Skip to main content
x
Uchambuzi wa athari za mabadiliko ya tabianchi na haki za ardhi Kwa wazalishaji wadogo

Uchambuzi wa athari za mabadiliko ya tabianchi na haki za ardhi Kwa wazalishaji wadogo

Mabadiliko ya Tabianchi ni mabadiliko ya hali ya hewa ya muda mrefu katika eneo fulani (Mkoa, Nchi au Bara) tofauti na iliyozoeleka. Mabadiliko hayo huleta athari katika nyanja za kiuchumi, kimazingira na kijamii. Mabadiliko ya Tabianchi ni tatizo linaliokabili dunia katika karne ya ishirini na moja na kutokana na athari zake katika nyanja mbalimbali zinazogusa maisha ya binadamu wa kawaida kila siku ikiwa ni pamoja na kilimo na ufugaji.

Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kitaifa, jitihada mbalimbali zinafanywa na mipango kadhaa inatekelezwa. Kadhalika Tanzania imeridhia na kutekeleza makubaliano ya kimataifa yenye miongozo ya kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi kulingana na jinsi nchi yetu ilivyobainisha katika mikakati ya kitaifa. Makubaliano hayo ni pamoja na UNFCCC na Mkataba wa Kyoto wa 1996 na 2002 ili kuhakikisha kuwa masuala ya mabadiliko ya tabia nchi yanaungwa mkono na Sera na Sheria za nchi.

Kupitia Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997, Tanzania imejiwekea mazingira mazuri katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Vilevile, kuna mipango na mikakati inayolenga kukabiliana na mabadiliko hayo, mfano Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi (2012) ambao unalenga kuiwezesha Tanzania kuhimili na kushiriki katika jitihada za kidunia za kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa mitazamo wa kufikia maendeleo endelevu. Mipango mingine ni Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2013) ambao unalenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwezesha ujumuishaji wa namna ya kuhimili mabadiliko katika sera, programu na mipango ya maendeleo.

Sababu za kutokea kwa mabadiliko ya tabianchi kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ni pamoja na vile vya kiasili pamoja vile vinavyotokana na shughuli za kibinadamu ambazo ni pamoja na uvunaji wa misitu usio endelevu kwa ajili ya biashara ya mbao na mkaa; Uvamizi wa misitu kwa ajili ya shughuli za kilimo, makazi, na ufugaji ambapo miti ya asili hukatwa; Uchomaji moto misitu na mbuga kwa ajili ya kurina asali, kuandaa mashamba na uwindaji wa wanyama wadogo ambayo hupoteza uoto wa asili na kutoa hewa ukaa; Ongezeko la viwanda duniani ambavyo mifumo yake ya uzalishaji na matumizi yake kama vile mitambo na magari hutoa hewa ukaa na kemikali zenye madhara katika tabaka la ozone; na Matumizi ya mbolea za viwandani katika kilimo.

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na hizi zifuatazo; uhaba wa maji kutokana na kukauka kwa vyanzo mbalimbali vya maji; Majira ya msimu ya mvua kutotabirika maeneo mengi nchini; Uharibifu wa miundombinu unaotokana na upepo mkali, mvua kubwa na mafuriko; Ongezeko la magonjwa (mapya na ya zamani) mfano malaria; Kutokuwa na uhakika au wasiwasi wa maisha. Hali hii huwakumba sana wakulima na wafugaji ambao mifumo yao ya uzalishaji imeathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi; Migororo ya ardhi baina ya watumiaji wa ardhi. Kupungua kwa rutuba na mvua katika maeneo mbalimbali nchini, kumesababisha makundi ya wakulima na wafugaji kuhama kwa ajili ya kupata malisho, maji na ardhi yenye rutuba; Kupanda kwa gharama za vyakula; Kumekuwa na ongezeko la bei za mazao ya chakula katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na ukubwa wa gharama za uzalishaji mfano pembejeo za kilimo kama mbegu zinazohimili ukame, uhitaji mkubwa wa mbolea na madawa pamoja na uhifadhi wa mazao; na upungufu wa uzalishaji wa chakula unaotokana na mabadiliko ya misimu ambayo hupelekea hali ya ukame au mvua kubwa ambavyo huharibu mazao.

Malengo ya uchambuzi huu uliofanyika tarehe 1 hadi 3 Machi 2021 ni pamoja na kuibua namna ambavyo mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri haki za ardhi hususani kwa wazalishaji wadogo ambao hutegemea majira na nyakati za mvua na jua katika kuendesha kilimo pamoja na ufugaji. Vile vile, uchambuzi huu unataka kubaini ni kwa namna gani mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi inavyoathiri haki za ardhi za wazalishaji wadogo nchini kwasababu kuna mikakati mingine inayopelekea makampuni ya uwekezaji kuchukua mashamba makubwa ambayo wakulima wadogo walitumia kupanda miti lakini wao huyageuza na kuwa ya kupanda miti. Uchambuzi huu pia utatazama sera na sheria zilizoanzishwa kwa lengo la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na namna ambavyo wazalishaji wadogo wameshirikishwa katika kutoa maoni yao ili mipango mbalimbali itakayotekelezwa kutokana na sera na sheria hizi zisiathiri haki za wazalishaji wadogo.

Uchambuzi huu ukikamilika utatumika katika kuibua mjadala kwenye jamii ili kuongeza uelewa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na haki za ardhi pamoja na kuwashirikisha watunga sera na sheria mapendekezo yaliyoibuliwa na uchambuzi huu na kutafuta namna ya kuboresha au kutunga sera na sheria zinazokidhi maslahi ya makundi yote.

ARDHI NI UHAI