Skip to main content
x
Maadhimisho ya siku ya wanawake na ukombozi wa wazalishaji wadogo.

Maadhimisho ya siku ya wanawake na ukombozi wa wazalishaji wadogo.

Historia ya siku ya Wanawake duniani inaonesha kuwa tarehe 8 Machi ilichaguliwa kusherehekea siku ambayo wanawake katika Urusi ya Usoviet walianza kufanya maandamano ya haki ya kupiga kura ambayo walipewa mnamo 1917. Kwa hiyo ni sahihi kusema kuwa chimbuko la siku ya wanawake iliadhimishwa tu na wanaharakati wa kijamaa na nchi za kikomunisti. Ilipofika miaka ya 1960 hususani mwaka 1967 vuguvugu kubwa la wanawake (Feminist movement) walianza kuitumia siku hii kuadhimisha siku ya wanawake. Mwaka 1975, Umoja wa Mataifa uliirasimisha siku hii kuwa siku ya Wanawake duniani hivyo kupata umaarufu mkubwa kutokana na kusherehekewa kwenye kila nchi ambayo ilikuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Kwa mwaka 2021 siku ya Wanawake duniani na hapa Tanzania inaadhimishwa leo tarehe 08.03.2021 ambapo ujumbe mahsusi wa siku hii ni “Wanawake katika uongozi chachu ya kufikia dunia yenye usawa”. Katika kusherehekea siku hii katika nchi yetu kumekuwa na pilika pilika na heka heka nyingi katika makundi, taasisi, vyombo vya habari na mitandao mbalimbali. Kuna mengi ya kujifunza katika kuadhimisha siku hii muhimu ambayo inatumika na wanawake kusema, kueleza, na kuandika masaibu yote yanayowasibu katika maisha yao katika nyanja za kijamii, kitaaluma, kiuchumi, kisiasa na hata kiteknolojia. Swali la kujiuliza tunapoadhimisha siku hii kama taifa ni kwa namna gani maadhimisho haya yanawagusa wanawake waliopo vijijini ambao ndio wazalishaji wakubwa katika mashamba na ufugaji.

Ni dhahiri kuwa wanawake waliopo pembezoni hawajui na wala hawana taarifa kuhusu uwepo wa siku hii katika kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha yao. Sio vibaya kuisherehekea siku hii kwenye kumbi kubwa za mikutano na wala sio vibaya kusherehekea kupitia mitandao ya kijamii, radio na televisheni bali ni muhimu sana kuhakikisha kuwa siku hii inamgusa mwanamke anaenyanyasika na mifumo isiyomruhusu kupata, kutumia na kumiliki mali ardhi ikiwa ni mojawapo.

Katika siku hii ujumbe mahsusi wa HAKIARDHI ni kuimarisha nafasi na nguvu ya mwanamke mmoja mmoja na wanawake kwa ujumla katika kupata, kutumia na kumiliki rasilimali ardhi na rasilimali nyinginezo. HAKIARDHI inatambua mchango mkubwa wa wanawake katika harakati za kutetea haki za ardhi kwa wazalishaji wadogo. Wanawake ndio wazalishaji wakubwa katika ardhi katika ardhi ya kijiji wakijihusisha na kazi mbalimbali za uzalishaji mali hususani kilimo na ufugaji. Wanawake katika vijiji vingi nchini ndio wanaolelea familia kwa kutumia ardhi kama nguzo kuu ya uchumi katika familia na jamii zao.

Rai ya HAKIARDHI kwa serikali ni kuweka mfumo mzuri ambao utawawezesha wanawake kuwa wanufaika wakubwa wa ardhi nchini. Tunapozungumza kuwa na wawekezaji katika ardhi za vijiji, wanawake wapewe kipaumbele kwa kuwa wana uwezo wa kuzalishaji mazao ya kutosha. Serikali iimarishe masoko ambayo wanawake wanaweza kuuza mazao wanayovuna ili waweze kupata faida ambayo wataiwekeza kwenye ardhi zao. Serikali isimamie mabenki ambayo sio ya kibishara ambayo yatawakopesha wanawake hawa pasipo kuwanyonya kupitia mikopo yenye riba kubwa na ya kinyonyaji.

Mchango wa HAKIARDHI katika utetezi wa haki za wanawake umekuwa ni pamoja na kutoa elimu ya haki za ardhi kwa wanawake pamoja na watoto wa kike katika shule za msingi na sekondari. Elimu hii ya haki za ardhi imewawezesha wanawake kuwa sehemu ya mapambano ya kijamii ya kutetea haki za ardhi kwa lengo la kuhakikisha kuwa wazalishaji wadogo kwa ujumla wake wanailinda na kuitumia ardhi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.