Madai ya wanavijiji wilaya ya kilosa kuhusu ugawaji wa mashamba
1. Utangulizi
Wilaya ya Kilosa iliyopo mkoani Morogoro ni moja ya wilaya zenye mashamba makubwa yanayofaa kwa kilimo na ufugaji. Kwa miaka mingi idadi kubwa ya mashamba haya yamekuwa yakimilikiwa na wawekezaji pamoja na watu wengine ambao si wanavijiji. Hali hii imepelekea migogoro ya ardhi ya mara kwa mara miongoni mwa watumiaji wa ardhi kutokana na kupambania ardhi kwa matumizi ya kilimo na ufugaji.
Kati ya mwaka 2017 hadi 2021 serikali kupitia mamlaka ya Rais ilifanya maamuzi ya kubatilisha na kufuta hati za umiliki wa baadhi ya mashamba ya wawekezaji ambayo hayakuendelezwa kwa muda mrefu. Lengo la kubatilisha umiliki wa mashamba hayo ni kuyarudisha kwa wakulima na wafugaji kwenye wilaya husika ambao ndio waliopaza kwa miaka mingi wakitaka kupatiwa ardhi ya kilimo na ufugaji. Ingawa utekelezaji wa lengo hili umekuwa na konakona nyingi kutokana na kuchukua muda mrefu zaidi pasipo wavijiji kufahamu hatima yao katika kupata ardhi kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya chakula. Kati ya mashamba 11 yaliyobatilishwa umiliki, mashamba 5 yapo kata ya Msowero (mashamba 2 yapo kijiji cha Mambegwa ambayo yalishakabidhiwa kwa kijiji na mashamba 3 yapo kijiji cha Msowero). Mashamba 3 ya kata ya Ulaya na 3 kata ya Kimamba yameingizwa katika mpango wa mashamba ya bloku unaosisitizwa na serikali.
Kumekuwepo na madai ya wanavijiji kuwa mashamba yaliyobatilishwa umiliki badala ya kurudishwa kwao kama walivyoahidiwa na serikali badala yake watendaji katika ngazi ya Wilaya, Kata na Kijiji wamekuwa wakiyakodisha mashamba hayo kwa wakulima kwa kila msimu. Pamoja na wanavijiji kulalamika mara kwa mara bado urejeshwaji wa mashamba haya haujafanyika ipasavyo badala yake kumekuwa na ahadi za michakato isiyo uwazi na isiyokamilika hivyo kuwaacha wanavijiji bila ya uhakika wa umiliki na matumizi ya ardhi wanayoitegemea katika kuzalisha chakula na kuendesha maisha kiuchumi na kijamii.
Mwaka huu 2022 serikali katika ngazi ya Wilaya walitoa maelekezo kwa vijiji vya Msowero na Majambaa na vijiji vingine kuhusu mpango wa kugawa mashamba yaliyobatilishwa umiliki wake katika vikundi vya watu wasiopungua 20 na wasiozidi 50 kwa kila kikundi kupewa bloku moja ya ardhi yenye ekari 50 kwa matumizi ya kilimo cha mazao ya kipaumbele ambayo ni mkonge na miwa. Mpango wa serikali kuyagawa mashamba kwa vikundi sio taarifa njema kwa wanavijiji kwa sababu tayari wanayatumia mashamba haya hata kabla ya ubatilishaji wa hatimiliki kutokana na kutelekezwa na wawekezaji kwa muda mrefu. Badala yake wanavijiji wanataka ardhi hizo zirudishwe kwenye mamlaka za vijiji, ambazo ni Halmashauri za Vijiji na Mikutano Mikuu ya Vijiji, ili wanavijiji wakubaliane wenyewe namna sahihi ya kugawiana ardhi hizo kwasababu ni ardhi za vijiji.
Mpango huu wa kugawa mashamba katika vikundi umeibua sintofahamu vijijini wilayani Kilosa, kwa sababu kuna vijiji vilivyokubaliana na mpango huu wakiamini kuwa angalau watarudishiwa ardhi yao na kuitumia pasipo kukodishiwa kila msimu. Kijiji kimojawapo kilichokubaliana na utaratibu huu ni kijiji cha Msowero. Lakini vilevile kumekuwepo na vijiji ambavyo vimepinga kwa nguvu zote kuunda vikundi hivi mojawapo ya kijiji hiki ni Majambaa. Kutokana na msimamo wa wanavijiji kukataa mpango huu kumekuwapo na matishio yanayotolewa na viongozi na watendaji wa wilaya na kata kwa wanavijiji na viongozi wao ambao wanataka serikali isikilize maoni na madai yao ya namna ambavyo wanataka ardhi zigawiwe kwao kwa matumizi ya kilimo na ufugaji.
2. Taratibu za Uundaji wa Vikundi
Ni dhahiri kuwa wanavijiji hususani wakulima wadogo hawakubaliani na ugawaji wa mashamba katika vikundi lakini wamelazimika kukubaliana na utaratibu huu ili kuepuka kuyapoteza kabisa mashamba hayo ikizingatiwa kuwa kumekuwa na matamko mbalimbali kutoka kwa viongozi wa ngazi tofauti kuwa mashamba hayo watapatiwa wawekezaji walio makini kuyaendeleza.
Katika vijiji vilivyokubali kuunda vikundi ni pamoja na kijiji cha Msowero, ambapo jumla ya vikundi 31 vyenye wakulima 20 hadi 50 vimeundwa. Maelekezo ya uongozi wa Wilaya kuhusu kuunda vikundi ni kama ifuatavyo; Kwanza, kikundi kiwe na wakulima wasiopungua 20 na wasiozidi 50; Pili, kikundi lazima kiwe na katiba inayoeleza kanuni za kuendesha na kuongoza kikundi, viongozi wa vikundi na majukumu yao; Tatu, kikundi lazima kisajiliwe na Afisa Maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa; Nne, kikundi lazima kiwe na akaunti ya benki; Tano, kila mwanakikundi lazima achange shilingi 3,000/= kwa matumizi ya uundaji na usajili wa kikundi; Sita, kikundi lazima kilipe shilingi 10,000/= za usajili kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa; Saba, kila kikundi lazima kipate namba ya usajili ambayo inatolewa na Wilaya kama utambulisho rasmi wa kuwezesha kugawiwa shamba la kilimo.
3. Changamoto katika Uundaji na Usajili wa Vikundi
Uundaji na usajili wa vikundi umegubikwa na changamoto nyingi ambazo zimewaingiza wanavijiji gharama na usumbufu. Changamoto hizi ni kama vile; Mosi, awali wanakikundi waliandaa katiba za vikundi vyao kwa mtazamo na mawazo yao lakini baada ya kuwasilisha katiba hizo kwa Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya waliambiwa kuwa katiba walizoandika hazifai na hazikidhi vigezo. Kwahiyo, Wilaya iliandaa katiba itakayotumika na vikundi vyote kwa kuweka taarifa chache tu kama vile jina la kikundi na majina ya viongozi wa vikundi lakini taarifa nyingine zote zilishaandaliwa na Wilaya. Malalamiko ya wanavikundi kuhusu utaratibu huu, ni kwa viongozi wa Wilaya kutokuheshimu mawazo yao katika kuunda katiba, vilevile ili kupata katiba hiyo kila kikundi kilitakiwa kuchanga shilingi 30,000/= ikiwa ni gharama za kuandaa katiba na kudurufu nakala, malipo haya hayana stakabadhi yoyote kwa sababu hulipwa kwenye steshenari zinakopatikana nakala za katiba iliyoandaliwa na Wilaya.
Changamoto nyingine ni kuanzishwa kwa vikundi ambavyo vinaundwa na watu ambao sio wanavijiji wa kijiji cha Msowero na Wilaya ya Kilosa bali wanajisajili kwa njia za panya kuwa wanavijiji na kujiingiza katika vikundi hivi ili kugawiwa ardhi. Hoja ya muhimu inayojengwa na wanavijiji ni kuwa kwa miaka mingi wamefanya harakati za kuiomba serikali ibatilishe umiliki wa mashamba haya ya uwekezaji lakini badala ya wao kupata kipaumbele katika kugawiwa ardhi badala yake wageni wanapewa kipaumbele.
Vilevile, vikundi hivi vimeundwa pasipo mwongozo wowote wa namna vitakavyojiendesha, namna gani vitatumia ardhi watakayopewa. Je, watalima kama kikundi au kama mtu mmoja mmoja? Je, vikundi hivi vitaendeshwa kama Ushirika, Vikoba au Saccos? Je, watalima na kuvuna na kuuza mazao kwa utaratibu gani? Matumizi ya maneno vikundi vya ujamaa na ushirika yanayotumika katika kuhamasisha na kuhalalisha ugawaji huo wa mashamba ni ulaghai kwasababu unatoa mwanya wa uporaji ardhi.
Changamoto nyingine ni vikundi kulazimishwa kulima mazao ya biashara tu ambayo ni mkonge na miwa. Amri hii imewatatiza wakulima kwa sababu haya sio mazao ya kipaumbele kwao bali wangependelea kulima mazao ya chakula ambayo wamekuwa wakiyalima kwa siku zote. Msimamo wa wakulima ni kuwa hawapo tayari kulima mkonge na miwa kwa sababu hawana ujuzi wa kulima mazao haya, hawajuhi hatima ya masoko kwa sababu hakuna maelezo yoyote kuhusu kuendeleza kilimo cha mazao haya zaidi ya kuambiwa kutaanzishwa viwanda vya uwekezaji vitakavyonunua malighafi kutoka kwa wakulima.
4. Ukakasi katika Ugawaji wa Mashamba kwa Vikundi
Mapema mwezi Oktoba 2022 ulifanyika uzinduzi wa ugawaji wa ardhi kwa vikundi ulifanyika katika kijiji cha Ilonga kata ya Chanzulu wilaya ya Kilosa ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Shaka Hamdu Shaka; Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mheshimiwa Fatma Abubakar Mwasa, viongozi wa chama tawala na viongozi wa vijiji na kata. Wakulima katika vikundi walipatiwa taarifa kuwa siku ya Ijumaa tarehe 14.10.2022 ndio ugawaji wa mashamba ungefanyika kwahiyo walitakiwa kujiandaa kwa zoezi hilo. Tofauti na matarajio ya wakulima ugawaji wa mashamba ulifanyika katika mashamba ambayo sio huyatumia kupitia kukodishwa badala yake waligawiwa mashamba mengine na walipohoji walijibiwa kuwa hakuna nafasi ya kuchagua shamba mnalotaka.
Tofauti na maelezo ya awali ya Wilaya ni kuwa kila kikundi chenye watu wasiopungua 20 na wasiozidi 50 kitapata bloku la shamba lenye ekari 50. Lakini katika hali ya kushangaza waliambiwa kuwa ni vikundi 16 tu katika vikundi 31 vilivyoundwa katika kijiji cha Msowero ndio vingepatiwa mashamba. Kwa maana hiyo vikundi vingine 15 vitalazimika kuvunjwa na kujazia watu katika vikundi vilivyopata ardhi, hivyo vikundi vingine kuwa na watu 100 na zaidi wakati ukubwa wa ardhi ni ule ule wa ekari 50.
Katika hali isiyotarajiwa katika zoezi la ugawaji wa mashamba kwa vikundi hakukuwepo na viongozi wa vijiji bali Maafisa kutoka Wilayani. Hali hii ilisababisha wakulima kukosa sehemu ya kulalamikia na walilazimika kukubali maelekezo yote waliyopewa kwasababu yaliambatana na vitisho kuwa haisyekubali utaratibu uliowekwa kikundi cha walalamishi hakitapata ardhi bali watapatiwa vikundi vingine vyenye mahitaji ya ardhi.
Vilevile, wanavijiji wanalalamika kuhusu mashamba ambayo yameshagawiwa kwa watu ambao sio wanavijiji wa vijiji husika kutokana na nguvu za kisiasa na kifedha. Kwa mfano, wanavijiji wa kijiji cha Msowero wanafahamu baadhi ya watu wenye zaidi ya ekari 200 ambazo ni sehemu ya mashamba yaliyotakiwa kugawiwa kwa wanavijiji. Hivyo, serikali inaposema kijiji cha Msowero kina ekari 1,769 zinazotakiwa kugaiwa kwa wanavijiji sio sahihi kwasababu kuna ardhi imeshagawiwa kwa watu binafsi ambao wengine ni viongozi na matajiri katika sehemu mbalimbali.
5. Madai na Mapendekezo ya Wavijiji Wakulima wa Kilosa
Wanavijiji katika vijiji vya Msowero, Majambaa na vijiji vingine wanahitaji kutambulika kama watumiaji wa asili wa mashamba haya kabla na hata baada ya kugawiwa kwa wawekezaji walioshindwa kuyaendeleza. Vile vile, ni wanavijiji waliopaza sauti na kufanya harakati za kutaka umiliki wa mashamba haya ubatilishwe. Halikadhalika, wanavijiji ndio waathirika wa migogoro ya ardhi kutokana na uhaba wa ardhi ya kilimo na ufugaji. Kutokana na sababu hizi, wanavijiji wana madai yafuatayo;
- Mashamba haya yagawiwe kwa wanavijiji ambao wamekuwa wakiyatumia mashamba haya kwa muda mrefu tena kwa kukodishiwa kila msimu kwa gharama kubwa. Hivyo basi, wanavijiji waachwe kwenye mashamba husika hata kama itabidi kuwekwa kwa kiasi cha ardhi ambacho kila mkulima atapata ili wapate wanavijiji wengi zaidi lakini sio kulazimisha vikundi.
- Mfumo wa uanzishwaji wa vikundi ufutwe kwasababu haueleweki na hauna tija kwa wanavijiji kwasababu hauoneshi ni kwa namna gani vikundi hivi vitawasaidia wao katika kuzalisha na kupata faida. Hii ni kwasababu uanzishwaji wa vikundi hivi ni shinikizo kutoka ngazi za juu na sio matakwa ya wanavijiji ndio maana hata mfumo wa kuendesha vikundi hivi haujulikani kama ni wa ushirika, vikoba au saccos.
- Wakulima hawapo tayari kutekeleza mpango wa kilimo cha mazao ya kipaumbele ambayo ni mkonge na miwa, kwasababu maamuzi hayo hayakuwa shirikishi na sio kipaumbele chao bali wakulima wapewe uhuru wa kulima mazao wanayoyataka na wenye uzoefu wa kuyalima kwa muda mrefu hususani mazao ya chakula.
- Wanavijiji wamilikishwe mashamba pasipo masharti yoyote ili wawe na uhakika na uhuru wa kuyatumia kwa kilimo pasipo bugudha au vitisho vya kunyang’anywa na mamlaka yoyote hapo baadae.