Wanawake kilolo wathubutu
Agnesi Kiwele wa Kijiji cha Ng'ang'ange, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa anasimulia alivyopigania mpaka wa shamba lao akisema,
Siku moja mwaka 2018 nilienda shambani kwetu, shamba alilotuachia marehemu baba yetu. Nilipofika shambani nilikuta baba mdogo ameweka mpaka tofauti na ilivyokuwa awali.
Kiukweli hakuwa na sababu za msingi ninachoweza kusema alikuwa ametawaliwa na tamaa na msukumo wa mila kandamizi, kwamba sisi watoto wa kike tulioachwa na wazazi wetu hatupaswi kumiliki ardhi. Mimi kama mwanamke niliamua kusimama imara kutetea haki yangu na ya mdogo wangu baada ya baba yangu mdogo kutaka kunyang'anya shamba.
Sikubishana naye, tukiwa pale shambani niliamua kwenda kwa mama yangu mkubwa kumpa taarifa kwamba nimeenda shambani nimekuta baba mdogo amepitisha mpaka katika shamba letu. Mama yangu mkubwa alimfuata kumuuliza, na alivyomuuliza baba mdogo alikiri kuingia katika shamba letu na akatuachia kipande cha shamba alichotaka kuchukua. Mimi nilikuwa nafikiri pale endapo angechukua maamuzi ya kukataa ningechukua hatua za kisheria kwani najua taratibu zilivyo na ninao uwezo na ujasiri wa kuchukua hatua.
Kwa sasa, mahusiano na baba yangu mdogo yapo vizuri kwani niliamua kumuomba msamaha kama nimemkwaza kwa kudai haki yangu, yeye alikiri kwamba kweli alifanya makosa na mimi nikaamua kumsamehe na sasa tunaishi vyema. Kiukweli sio kitu kilichozoeleka na wala kwangu haikuwa jambo jepesi kama mtoto wa kike kuhoji maamuzi ya baba mdogo. Nilijipa moyo na niliuvaa ujasiri kutokana na uwelewa wa taratibu za umiliki wa ardhi na haki za ardhi kwa wanawake.Natamani kuona dunia yenye wanawake wengi wanaojiamini na kulinda haki zao bila woga wowote.
Mimi kama mwanamke nilichukua maamuzi hayo Ili mwanamke mwingine aweze kujifunza kupitia mimi.